USHINDI wa Chadema katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata tatu za
udiwani, umezidi kukiweka pabaya, CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,
huku sababu za ushindi huo zikitajwa kuwa ni matumizi mazuri ya kasoro
za chama hicho tawala katika mambo mbalimbali.
Chadema kimepata
ushindi katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki baada ya mgombea
wake, Joshua Nassari kuwashinda wenzake saba katika kinyang’anyiro
hicho.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii kwa
chama cha upinzani kushinda uchaguzi mdogo katika jimbo ambalo kabla
halijawa wazi kwa sababu zozote zile, lilikuwa mikononi mwa CCM.
Arumeru
Mashariki limekuwa wazi tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya aliyekuwa
mbunge wake, Jeremia Sumari (CCM), kufariki dunia.
Nassari
ameshinda kwa asilimia 54.91 wakati mpinzani wake wa karibu, Sioi Sumari
wa CCM alipata asilimia 44.56 ya kura halali 60,038 zilizopigwa katika
vituo 327 vya kupigia kura.
Sababu za ushindi
Chadema
kiliingia katika kinyang’anyiro hicho kwa kujishusha hivyo kupata muda
wa kujifunza jinsi ya kwenda kuishi na wananchi wa Arumeru kwa maana ya
kufahamu lugha ya kuzungumza nao, kutambua mahitaji yao, kisha kutafuta
majawabu ya kuwapa juu ya mahitaji hayo.
Kilijenga timu imara ya
kuratibu kampeni zake kwa ufanisi, na jukumu hilo liliangikia kwa watu
watatu, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse na Meneja mwenza wake,
Vicent Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini na Mkurugenzi wa
Masuala ya Bunge, John Mrema ambaye alipewa jukumu la kusimamia
oparesheni zote.
Nyerere pia alichukuliwa kama kete ya Chadema
kuwashawishi wananchi wa Arumeru ambao wanaaminika kuwa waumini wa siasa
za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kupata uthibitisho kwamba hata
katika familia yake, wapo watu wa upinzani.
Licha ya CCM kutuma
timu nzito ya vigogo katika kampeni zake, Mwenyekiti na Rais Mstaafu,
Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, Mlezi wa CCM Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uratibu na
Uhusiano, Stephen Wassira, Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama na Katibu wa
Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye bado mgombea wake aliangushwa.
Hata
hivyo, uchaguzi huo umefanyika wakati CCM kikiwa katika mpasuko mkubwa
ambao umechangiwa na siasa za makundi. Makundi hayo ni ya vigogo wa
chama hicho, ambao wanajipanga kuwania Urais mwaka 2015 na kwa sasa kila
kundi linaendesha mipango wa kujiimarisha katika kila eneo muhimu
kuanzia ngazi za chini.
Ishara za kushindwa
Ishara za kushindwa
CCM zilianza kuonekana katika mchakato wa mwanzo wa kura za maoni ndani
ya chama hicho, kwani wanachama ambao walijitokeza kugombea na
kushindwa, wengi wao hawakuvunja kambi zao.
Makundi yaliyokuwa na
nguvu ni yale yaliyokuwa na makada wa chama hicho, William Sarakikya,
Elirehema Kaaya na Elishiria Kaaya ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu (Nec) ya CCM Mkoa wa Arusha.
Pia siasa za makundi ndani ya CCM
Mkoa wa Arusha, ambako bado vigogo wa chama hicho, hasa Katibu wa Mkoa,
Mary Chatanda na Mwenyekiti wake, Onesmo Nangole hawana uhusiano mazuri
kunaelezwa kuwa ni moja ya sababu za kuanguka.
Awali, Chatanda ambaye
anadaiwa kuwa na mgogoro na wana-CCM wengine wa Arusha, alitajwa
kumpinga waziwazi Sioi katika kura za maoni na alimpa karata yake
Sarakikya na Elishilia Kaaya ambao wote walishindwa.
Pia wanasiasa waliotumika katika kampeni za CCM katika uchaguzi huo mdogo ni moja ya mambo ambayo yalikiathiri chama hicho.
Lugha
zilizokuwa zikitumiwa na baadhi yao dhidi ya viongozi wa juu wa Chadema
na wabunge wake kwa mfano, alizokuwa akimwaga jukwaani, mpiga kampeni
nguli wa wake, Livingstone Lusinde ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM (Nec), ni moja ya mambo yanayooelezwa kuwa yalichangia
kupunguza kura za mgombea wa chama hicho.
Pia kuhujumiana ndani ya
chama kwa kuvujisha taarifa za vikao vya siri vya mikakati ya ushindi,
kiasi kikubwa kumechangia chama hicho kushindwa kwa tofauti ya zaidi ya
kura 6,000.
Moja ya mambo ambayo yanadaiwa kutoka ndani ya CCM, ni
siri ya kuongeza vituo vya kura, mpango wa kubadilishwa baadhi ya
matokeo ya fomu za mawakala, kuingizwa kura bandia kupitia mabalozi wa
nyumba kumi katika vituo mapema alfajiri na pia, kuhongwa kwa baadhi ya
mawakala.
Mipango hiyo inadaiwa kukwama hata kabla ya siku ya kupiga kura hali ambayo inadaiwa kuwa iliichanganya kambi ya CCM.
Hata
katika upangaji wa ratiba ya kampeni na wazungumzaji katika kampeni
hizo, kunadaiwa kulikuwa na hujuma miongoni mwa wazungumzaji huku kundi
moja likituhumiwa kufika katika jimbo hilo, kuhujumu kampeni kwa kutoa
lugha ambazo haziwapendezi wananchi na hivyo kuwachukiza.
Sababu
nyingine ni gtuhuma za ufisadi zinazowakabili baaadhi ya makada wa chama
hicho. Hilo limewafanya baadhi ya wananchi kukichukia wakiamini kuwa
mafisadi ambao hupigwa vita na Chadema ndiyo chanzo cha umaskini mkubwa
unaowakabili Watanzania.
Kampeni
Uzinduzi wa kishindo wa
kampeni za chama hicho ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha
Televisheni cha Star, Machi 10, mwaka huu uliashiria kwamba Chadema
kilikuwa kimedhamiria kushinda.
Mbali na shamrashamra za hapa na
pale, mkutano wa uzinduzi ulipanga ajenda za kampeni za chama hicho na
aliyekuwa mgombea, Nassari na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe
waliweka bayana kwamba suala la ardhi ni miongoni mwa mambo ambayo
yatapewa umuhimu mkubwa.
Ajenda nyingine ambayo pia iliwekwa
wazi na Nassari ni matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jimbo hilo
ambalo kuna chanzo kikuu cha maji kwa Miji ya Arusha na Monduli.
Ajenda
hizo za ardhi, maji na nyingine pia zilibebwa na timu za kampeni
wabunge wa chama hicho ambao walikuwa wakifika nyumba hadi nyumba mbali
na mikutano ya hadhara vijijini.
Matumizi ya helkopta katika siku
tisa za mwisho za kampeni, yalimwezesha Nassari na timu yake ya kampeni
kuwafikia wananchi wengi zaidi katika muda mfupi sambamba na kuongeza
hamasa kwa maana ya kuwa sehemu ya kushawishi watu kufika kwenye
mikutano katika sehemu mbalimbali.
Viongozi wakuu wa Chadema,
Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa walikuwa na
mchango mkubwa katika kufanikisha ushindi wa Nassari.
Kulikuwa na
kila dalili kwamba viongozi hawa wanakubalika na kuaminika kwa wananchi
kwani kila walipofika na kuhutubia, idadi ya watu ilikuwa kubwa na
utulivu ulionekana kuwa wa hali ya juu.
Uwepo wa viongozi hao
ulimwongezea nguvu kubwa mgombea wao ambaye pia alionekana kuwa na uwezo
mkubwa wa kujieleza akitumia lugha rahisi kuzungumzia matatizo
yanayowagusa watu katika eneo husika.
Ni kama alikuwa amefanya
utafiti wa kila alikokweda, kwani hotuba katika kijiji kimoja haikuwa na
uhusiano na hotuba ambayo angeitoa katika kijiji kilichofuata.
Kauli
za mgombea huyo kuhusu maisha duni ya watu hasa kina mama ambao
wamekuwa wakitozwa ushuru kwenye magulio, kukemea uonevu unaofanywa na
walowezi kwenye mashamba makubwa na kuzungumzia kwa ufasaha mahitaji
mengine ya wananchi kulimfanya kueleweka kwa urahisi kwa watu wa
kawaida.
Lakini pia Nassari alikwepa kuingia kwenye mitego ya
kujibu tuhuma mbalimbali zilizorushwa kwake na wapinzani wake hasa CCM
na mara zote alikuwa akisema: “Mimi namwachia Mungu.”
Nassari
aliingia kwenye uchaguzi huo kwa mara ya pili baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 31, 2010 ambako alipambana na marehemu Sumari na kupata kura
zaidi ya 19,000.
Udhaifu wa CCM
Timu ya kampeni ya Chadema ilimsaidia Nassari kutumia udhaifu wa CCM katika kufanikisha malengo yake.
Siasa
za matusi majukwaani ambazo baadhi ya wapiga debe wake walizitumia
hazikupata majibu kutoka Chadema na badala yake, Nassari alitumia msemo:
“Tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu.”
Majibu ya baadhi ya
tuhuma dhidi ya Chadema na mgombea wake yaliyotolewa na watu ambao si
sehemu ya chama hicho yalikijenga zaidi. Mathalan, Kanisa Katoliki
lilitoa tamko kwamba halijawahi kumtuhumu Dk Slaa kuhusu wizi wa fedha
kama ilivyodiwa na CCM.
Mengine ni kauli ya mtoto wa kwanza wa
Hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere kwamba Vicent Nyerere ni ndugu
yao tofauti na madai ya Rais Mstaafu Mkapa kwamba hakuwahi kumfahamu,
huku wazazi wake Nassari wakijitokeza jukwaani kupinga kile kilichosemwa
na Wassira kwamba mgombea huyo wa Chadema hakuwa na baraka za wazazi
wake kugombea nafasi hiyo.
Kauli hizo ziliwafanya makada wa CCM
waonekane kuwa si wa kweli mbele ya umma na hata yaliyosema baadaye
yalichukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni uzushi na uongo.
Maoni ya wadau
Wasomi na wanasiasa nchini wamesema ushindi huo wa Chadema ni fundisho kubwa kwa CCM kwamba watu sasa wanataka mabadiliko.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema huo ni
ushindi mkubwa kwa wananchi wanaopenda mabadiliko.
“Hii ni
ishara kwamba watu wanaotaka mabadiliko hapa nchini watawashinda watu
wasiotaka mabadiliko, Arumeru Mashariki ni sehemu tu ya mabadiliko
hayo,” alisema Dk Mkumbo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Alisema
hata kwenye chaguzi nyingine za kata katika Mikoa ya Mwanza, Mbeya na
Tanga wananchi wameonyesha kuwa wanataka mabadiliko.
Mkurugenzi
wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea
Nkya alisema wananchi wa Arumeru Mashariki wameipelekea CCM ujumbe
kupitia masanduku ya kura.
“Wamekiambia chama tawala kupitia ujumbe
wa kura kwamba hawaridhishwi na hali ngumu ya maisha wanayoishi hivi
sasa,” alisema Nkya.
Alisema wananchi hao wamechoshwa na ahadi za
uongo ambazo zimekuwa zikitolewa kila baada ya miaka mitano na sasa
wanataka mabadiliko.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro
alikipongeza Chadema na kusema kwamba uchaguzi huo unaonyesha kwamba
wananchi hivi sasa wanataka mabadiliko.
Hata hivyo, Mtatiro alisema
wakati umefika sasa kuweka utaratibu wa kuzuia uwepo wa chaguzi ndogo
kwa sababu zinatumia fedha nyingi za walipakodi.
“Tuandae
utaratibu wa kuachana na chaguzi ndogo zinatumia fedha nyingi. Wenzetu
Msumbiji na Ghana wameacha mfumo huo, mbunge anapofariki chama kinatoa
mbunge mwingine bila ya kuitishwa kwa uchaguzi,” alisema.
Kwa upande
wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema ni
vyema vyama vilivyoshinda na kushindwa vikafanya utafiti ili kufahamu
nini cha kufanya hapo baadaye.
“Hata chama kilichoshinda ni vizuri
kikafanya utafiti wa kwa nini kimeshinda uchaguzi huo ili kiweze
kuendeleza sababu hizo za kushinda,” alisema.
Alisema ni vyema
utafiti ukafanyika ili kufahamu ni kwa nini hivi sasa katika mfumo wa
vyama vingi idadi ya wananchi wanaopiga kura ni ndogo.
“Wakati wa
mfumo wa chama kimoja watu wengi walijitokeza kupiga kura kuliko sasa
katika mfumo wa vyama vingi ni lazima tufahamu kwa nini?”
Mkutano wa shukrani
Jana,
maelfu wa wakazi wa Arumeru Mashariki, walijitokeza katika mkutano wa
uliofanyika kwenye Uwanja wa Leganga ambao chama hicho kilizindulia
kampeni zake, kumpongeza Nassari kwa ushindi huo.
Mamia ya watu,
wengi wao wakiwa vijana walitembea kwa miguu hadi uwanja ni hapo
wakitokea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na Arusha Mjini.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mbowe aliwashukuru wakazi wa jimbo hilo, kwa imani
kubwa na heshma waliyokipa chama chake kwa kumchagua, Nassari kuwa
mbunge wao.
"Tunajua mlipata shida nyingi, mmekanwa sana,
mmepigwa mabomu, mmekamatwa lakini mkasema lazima mtamchagua kijana wenu
kuwa mbunge,”alisema.
Aliwataka vijana wenye shahada kuzitunza kwa
ajili ya uchaguzi ujao na wale ambao hawana wahakikishe wakati wa
kujiandikisha kwenye daftari jipya wanajitokeza.
Kwa upande wake,
Nassari alisema mara baada ya kutagazwa mshindi asubuhi, baada ya
dakika 15 tu, alianza kazi ya kuhakikisha vijana waliokuwa wamekamatwa
na polisi wakisherehekea ushindi wake wanaachiwa.
Imeandikwa na Neville Meena, Peter Saramba na Musa Juma, Arumeru na Raymond Kamnyoge, Dar.