Matokeo yasiyo rasmi kutoka Tanzania , yanaonyesha kuwa baadhi
ya wanasiasa wakongwe au vigogo wa chama tawala cha CCM wamepigwa kumbo katika
kura za maoni kuchagua wabunge ndani ya chama hicho.
Mchakato huo mkali uliofanyika siku ya Jumapili umesababisha kuanguka kwa John Malecela, aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM
Wabunge sita nje mkoa mmoja
Mkoa wa Iringa umeshuhudia wabunge sita wakishindwa kutetea viti vyao, katika
jimbo la Njombe Kaskazini, Jackson Makweta ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka
1970, ameangushwa na mfanyabiashara Deo Sanga. Bw Makweta aliwahi kuwa waziri
miaka ya nyuma.Kigogo mwingine aliyepokonywa heshima ya ubunge Joseph Mungai - jimbo la Mufindi Kaskazini, aliyewahi kuwa waziri wakati serikali ya rais wa kwanza, Julius Nyerere.
Wengi walioangushwa ni Profesa Raphael Mwalyosi (Ludewa), Benito Malangalila (Mufindi Kusini), Yono Kevela (Njombe Magharibi) na Monica Mbega (Iringa Mjini).
Anna Tibaijuka aliyekuwa msaidizi wa katibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na makazi, alimpiga mweleka
Mawaziri
Aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Diodorus Kamala
ametupwa katika kura za maoni kuwania jimbo la Nkenge.Baadhi ya Mwaziri waliokabiliwa na upinzani lakini wamepita ni Profesa David Mwakyusa (Afya) na John Chiligati (Ardhi).
Sura za vijana
Miongoni mwa sura mpya ni kijana January Makamba aliyemwangusha William
Shelukindo, mbunge anayemaliza muda wake jimbo la Bumbuli na kigogo wa CCCM.Vile vile yupo mtangazaji wa VOA ya Marekani, Juma Nkamia ameshinda maoni jimbo la Kondoa Kusini baada ya kumwangusha mwanasiasa mkongwe Pascal Degera.
Mwingine ni mwandishi wa habari, Deo Filikunjombe, aliyemtosa Profesa Mwalyosi wa jimbo la Ludewa.
Matokeo rasmi yatapatikana hivi karibuni, ingawa hata walioshinda hawana uhakika asilimia 100 wa kuwakilisha Chama Cha Mapindunzi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Wote watalazimika kusubiri kikao cha Kamati Kuu ambacho kina mamlaka na idhini ya kufuta wagombea watakaobainika kuwa wamekiuka taratibu za chama hicho - ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa kwa wapiga kura, jambo ambalo limedaiwa kujitokeza mara nyingi katika mchakato wa kura za maoni.
Kamati Kuu itakutana tarehe 14 Agosti.
No comments:
Post a Comment