Tuesday, April 3, 2012

Chadema yaibwaga CCM Arumeru 

 NI Chadema. Tambo za muda mrefu za nani angeibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki zilifikia kikomo jana, baada ya Chadema, kunyakua jimbo hilo.    Mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari aliibuka kidedea baada ya kupata kura 32,972 sawa na asilimia 54.91 ya kura halali 60,038 zilizopigwa katika vituo 327 vya kupigia kura jimboni humo.

Nassari alimbwaga aliyekuwa mshindani wake wa karibu, Sioi Sumari wa CCM, ambaye alipata kura 26,757 ambazo ni sawa na asilimia 44.56. Uchaguzi huo mdogo ulifanyika kufutia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari mwanzoni mwa mwaka huu.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi alisema watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 127,455 na waliojitokeza kupiga kura ni 60,699 sawa na asilimia 48.38 ambapo kura 661 zilikataliwa hivyo kufanya kura halali ziwe 60,038. 

“Kwa mujibu wa sura 343 ya sheria za uchaguzi nchini na kwa mamlaka niliyopewa namtangaza ndugu Nassari Joshua, kuwa mbunge wa jimbo hili la Arumeru Mashariki,”alisema Kagenzi, kauli ambayo iliibua shangwe kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wakisubiri matokeo hayo usiku kucha kwenye kituo cha kujumlishia kura kilichopo katika mji mdogo wa Usa River. 

Kagenzi aliwataja wagombea wengine ambao kwa ujumla wao walipata asilimia 0.53 ya kura zilizopigwa kuwa ni Abdalah Mazengo wa AFP aliyepata kura 139, Mohamad Abdalah Mohamed wa DP kura 77, mgombea wa SAU  Shabani Kirita aliyepata kura 22, Hamis Kieni wa NRA kura 35, wa TLP Abraham Chipaka kura 18 na mgombea wa UPDP, Charles Msuya alipata kura 18. 

Idadi ya wapigakura waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo mwaka huu waliongezeka kwa asilimia 8.2 ikilinganishwa na wapigakura 55,698 waliojitokeza Oktoba 31, 2010 kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.Kadhalika kura zilizokataliwa zimepungua kutoka za mwaka juzi kura 1,297 hadi kufikia kura 661 katika uchaguzi wa juzi, sawa na asilimia 49.03. 

Sioi, wenzake wakacha kusaini

Mgombea wa CCM, Sioi na wagombea wengine wawili wa vyama vya NRA na UPDP jana hawakujitokeza kusaini fomu za matokeo ya uchaguzi huo licha ya kuitwa mara kadhaa na msimamizi wa uchaguzi.  

Awali Sioi, alifika katika chumba cha majumuisho ya kura saa 6:15 usiku akiwa ameandamana na Makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Beno Malisa na makada kadhaa wa CCM na mara baada ya kufika katika chumba hicho, walifanya mazungumzo kidogo na msimamizi wa uchaguzi.
 

Baadaye Sioi aliondoka na makada hao majira ya saa 7 usiku na kutokomea huku Malisa akieleza kuwa mgombea huyo wa CCM jana hakuwa tayari kutoa maoni kuhusu uchaguzi huo.“Tunaomba mtuache kwanza, ila katika siasa kuna kushinda na kushindwa na mwanasiasa lazima atambue haya mawili,” alisema Malisa. 

Mkesha wa kusubiri matokeo
Wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kusubiri kwa saa zaidi ya 12 kwenye kituo hicho cha kuhesabia kura hadi saa 12.50 alfajiri ya jana wakati Kagenzi alipotangaza matokeo hayo.
 
Usiku huo ulikuwa ni wa taabu kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kati ya saa 8.00 usiku na saa 12.00 alfajiri huku kukiwa na katizo la umeme kwa zaidi ya mara mbili hivyo kukatiza mara kadhaa mchakato wa kujumlisha kura.Mvua hiyo ni kubwa ya kwanza kunyesha katika Wilaya ya Meru tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo mdogo Machi 9, mwaka huu hadi juzi wakati kura zilipoanza kujumlisha.
  
Maandalizi ya jenereta ya dharura yaliyokuwa yamefanywa na ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi, yaliwezesha kazi hiyo kuendelea hadi mchakato mzima ulipokamilika, hivyo kuwezesha mshindi kutangazwa saa 12.54 jana alfajiri.
 
Masanduku ya kura na fomu za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura vilianza kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi saa 1.20 usiku wa juzi na ilipotimu saa 7.00 usiku jana, tayari kata zote zilikuwa zimewasilisha taarifa zake. Hata hivyo kasoro iliyojitokeza ni pale polisi walipolazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana wakishangilia ushindi kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo.
 
Kati ya saa 2.00 na saa 4.30 usiku, mabomu hayo ya machozi na ya vishindo yalirindima mfululizo katika eneo la Usa River na kusababisha maduka, migahawa na baa kufungwa mapema.
 
Baadhi ya wafuasi wa Chadema walikamatwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema walikuwa na mpango wa kwenda kuwawekea dhamana katika Kituo Kikuu cha Arusha mjini ambako waliwekwa mahabusu.
 
Habari zinasema katika tafrani hiyo, gari la Mkuu wa Operesheni ya Polisi katika Uchaguzi wa Igunga, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Issaya Mngulu lilivunjwa kioo chake baada ya kupigwa na jiwe kutoka kwa waandamanaji.
  
“Hicho ni chanzo cha hasira za polisi ambao walirusha mabomu ya machozi kudhibiti hali hiyo maana tusingefanya hivyo hali ingekuwa mbaya zaidi,”alisema mmoja wa viongozi wa vikosi vya polisi ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa gazetini.

No comments: