Wabunge: Tulicharangwa mapanga mbele ya polisi
Joseph Zablon
WABUNGE wawili wa Chadema ambao walijeruhiwa kwa
mapanga na mashoka katika uchaguzi mdogo wa udiwani Jimbo la Kirumba,
Mwanza wamesema walipata kipigo hicho mbele ya polisi.
Wakizungumza
jana katika Chumba namba 310, Wodi 16 Jengo la Kibasila, Hospitali ya
Taifa Muhimbili, wabunge hao walidai kuwa walipigwa na vijana wa CCM
ambao walikuwa na watu wanaowatambua huku polisi wa doria wakishuhudia.
Mbunge
wa Ilemela, Highness Kiwia alisema kilichotokea hakukitarajia na
haamini kama polisi wanaweza wakashirikiana na majambazi kujeruhi
wengine.
“Nilipofika Ibanda Kabuhoro, kuna gari lilikuwa mbele
yangu likasimama, wakashuka watu kama 19 hivi, wakavunja kioo cha mbele
cha gari langu. Kuna polisi alikuwa amebeba silaha jirani akasogea,
nilipojaribu kufungua kioo kuzungumza naye nikapuliziwa ‘spray’ ambayo
siitambui,” alisema.
Kiwia alisema watu hao walikuwa
wakiwashambulia huku polisi wakiangalia… “wakati wote walitaka nitoe
silaha ambayo walidai kuwa ninayo huku wakinipiga na walianza kwa
kunipiga na rungu jichoni na kisha nikavutwa hadi nje ya gari na
kukanyagwa usoni.”
Mbunge huyo alisema watu hao waliendelea
kumpiga licha ya jitihada zake za kuomba msaada kwa polisi hazikuzaa
matunda na hata alipojaribu kushika suruali ya polisi ili ajinusuru kwa
kipigo, hakufanikiwa na ghafla alipigwa na kitu kizito kichwani.
“Fahamu
zilinivurugika, nilijikokota hadi katika gari la doria la polisi na
wakati najaribu kupanda polisi mwingine mwenye bunduki begani alinibeba
na kunitupa garini,” alisema Kiwia na kuongeza kwamba ndani ya gari hilo
aligundua kuwa ametupwa juu ya mwili wa Mbunge mwenzake, Salvatory
Machemli.
Alisema hayo yakitokea alipokuwa akielekea eneo la
Magnum ambako walielezwa kuwa kuna wana CCM ambao wamejikusanya sehemu
ambako aliambiwa kuwa huenda walikuwa wanagawana rushwa.
Hata
hivyo, alisema alipofika Ibanda gari lililokuwa mbele yake lilisimama…
“Ile barabara ni nyembamba hivyo nikawa nasubiri, ghafla wakashuka watu
kama 19 na mara gari jingine likaja na kusimama nyuma ya la kwangu, hofu
ikaniingia nikapiga simu kwa Wenje (Mbunge wa Nyamagana Chadema) ambaye
hata hivyo, simu yake ikawa haipatikani.”
Mbunge huyo alisema
alimpigia pia Machemli ambaye alipokea na kumweleza kuwa ametekwa na pia
akaifahamisha pia polisi lakini, akiwa bado amezungukwa na watu hao
gari la Machemli lilifika eneo la tukio na lilizingirwa na wahalifu hao
ambao pia walimpatia kipigo.
“Muda mfupi baadaye polisi walifika
na wawili kati yao wakiwa na silaha za moto na mmoja wao alisimama
jirani na mlango wa gari langu,” alisema na kuongeza kuwa ghafla kioo
cha mbele cha gari lake kilivunjwa.
Alisema kuona hivyo alishusha
kioo ili azungumze na polisi aliyekuwa amesimama jirani na gari lake,
wakati huo mbunge mwenzake akiendelea kunyukwa lakini mbele ya polisi
huyo.
“Walinishusha wakaanza kunipiga na walianza kwa kunipiga na
rungu jichoni, kisha mabapa ya mapanga, nikalimwa shoka kichwani na
kudondoka chini. Waliendelea kunipiga huku wakinikanyaga,” alisema.
Muuguzi wa wodi hiyo, Ezelina Zambi alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri.
“Kiwia
alipiga x-ray kifuani na kichwani na anasubiri kipimo cha MRI ili kujua
kama tissue za ubongo wake zimepata athari zozote,” alisema na kuongeza
kuwa kama kipimo hicho kitaonyesha hakuna tatizo huenda akaruhusiwa.
Wabunge
hao wawili walishambuliwa usiku wa kuamkia juzi na watu hao
wasiojulikana na baada ya tukio hilo walipelekwa katika Hospitali ya
Rufaa Bugando, Mwanza kabla kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Kiwia
na mwenzake pamoja na watu wengine kadhaa walishambuliwa na wanaodaiwa
kuwa ni wafusi wa CCM, hivyo kumsababishia majeraha kichwani.
Mbali
wabunge hao wengine ni waliojeruhiwa ni Ahmed Waziri ambaye anadaiwa
kuwa ni kada wa UVCCM aliyekatwa kiganja chake cha mkono wa kulia, Haji
Mkweda (21), Judith Madaraka (26) na Ivory Mchimba (26).
Alipoulizwa
jana kuhusu madai ya wabunge hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Liberatus Barlow alikataa kuzungumzia tukio hilo kwa maelezo kwamba
polisi bado inaendelea na uchunguzi.
“Tunafanya uchunguzi, kwa sasa hata majina haya ya majeruhi ambao niliwapa unaona hayajabainisha nani ni nani,” alisema.
No comments:
Post a Comment